AJTC

Saturday, 24 December 2016

Basata yaonya disko toto, maonesho machafu

Saturday, December 24, 2016

Basata yaonya disko toto, maonesho machafu



BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), linalosimamia sanaa na burudani nchini, limeonya wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani, kuepuka kuruhusu disko toto na kujaza watu kwenye kumbi hizo.

Aidha, Baraza hilo pia limesisitiza kuwa halitafumbia macho ukumbi utakaokiuka maelekezo yake, ikiwa ni pamoja na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu hasa yanayoonesha maungo ya ndani, kwa kuwa yameshapigwa marufuku.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, kwa lengo la  kuwatakia wasanii na wadau wote wa sanaa heri ya Krismasi na Mwaka mpya.

Huku ikisisitiza kauli mbihu yake kuwa ‘Sanaa ni kazi tuikuze, tuilinde na kuithamini’, Basata iliwataka wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani, kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizo kwenye vibali vyao vya uendeshaji kumbi.

“Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa matumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalumu hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao,” ilieleza taarifa hiyo.

Basata pia iliwakumbusha wamiliki wa kumbi za sherehe na burudani, kuwa inakatazwa kukusanya watoto kwenye kumbi hizo kupitia ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.

“Uzoefu unaonesha, kwamba nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi hujisahau na kuandaa madisko toto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

“Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida bila kujali maelekezo ya vibali vyao, wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na Basata,” ilieleza taarifa hiyo na kuonya kuwa hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka maagizo hayo.
 
 

Saturday, December 24, 2016

Mbowe Aeleza kwa nini Amekuwa Kimya Kupotea kwa Ben Saanane



Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amekuwa kimya muda mrefu kuhusiana na kupotea katika mazingira ya kutatanisha, msaidizi wake Ben Saanane kwa kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi. 
Mbowe alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa. 
Alisema yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake na ndugu wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu yake. 
“Ndugu zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea wale ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema Mbowe. 
Alisema, “Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake.” 
Katika hatua nyingine, Mbowe aliishitumu Serikali akidai kwamba imeendelea kuwafunga wanachama wake na kwamba mpaka sasa 180 wapo mahabusu. Alisema hizo ni jitihada za kuua nguvu za upinzani. 
Akijibu madai hayo, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani alisema jeshi hilo linawashikilia watu wengi kwa makosa mbalimbali vituoni na wengine mahabusu katika magereza. Alisema polisi haimkamati mfuasi wa chama cha siasa bali mtu anayekwenda kinyume cha sheria. 
“Hayo yanayosemwa siyo ya kweli, waache kulipaka tope jeshi la polisi. Tutaendelea kuwakamata watu wote wanaovunja sheria. Hata kama akiwa mjomba wangu tutamkamata.” 
Msigwa kidedea 
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliibuka kidedea baada ya kushinda kwa kupata kura za ndiyo 62 sawa na asilimia 58.49 kati ya kura 106 zilizopigwa. 
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Sadrick Malila ambaye alipata kura za ndiyo 93 sawa na asilimia 88 ya kura zilizopigwa 106 huku kura tatu zikiharibika. 

Mnyika alisema kuwa nafasi ya  mweka hazina imechukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ambaye alishinda kwa kupata kura 91 ambayo ni sawa na asilimia 86 kura zote 106 zilizopigwa. 
Mnyika alisema katika uchaguzi huo wajumbe walipiga kura za ndiyo au hapana kwa lengo la kufanya uchaguzi wa maridhiano kwani uchaguzi wa kuweka wagombea wawili husababisha makundi na kuleta migogoro ndani ya chama. 
“Hivyo Kamati Kuu Taifa baada ya kuliona hilo tukaamua kuwaita wagombea wote na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na hatujafanya huku tu, hata kanda nyingine tulizopita tumefanya hivyo" Alisema Mnyika
 
 

Saturday, December 24, 2016

Kingunge Asema Bila tume huru Wapinzani Wasahau Kuingia Ikulu .......Lowassa Akubali Yaliyopita Si Ndwele



Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kauli ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.

Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.

Mbali na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina wafanyakazi wake kote nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.

Kingunge, aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika siasa na jinsi alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema hali ya sasa ni mbaya kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao walikujwa wakali, kwa sababu CCM haifuati Katiba wala sheria.

“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.

Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya waziri anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na mkuu wa mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa sana.”

Alisema pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni vigumu kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa.

“Tufanye yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka mabadiliko,” alisema.

Alisema enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa nguvu na wengine, na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na kujiunga na Tanu kupigania uhuru.

“Tulifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu waliacha kazi, mtu anamaliza chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia Tanu kusaidia. Kwa hiyo tukawa na jeshi kubwa la vijana waliohakikisha nchi inapata uhuru,” alisema.

“Ninyi mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana katika mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine hawakufanya lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda kuitumikia Tanu. Miezi sita hatukuzungumza.”

Akizungumza mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwatia moyo vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, akisema bado jeshi kubwa la vijana linahitajika.

“Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema unakwenda mahali pengine, mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako. Nimefurahia moyo huo. Kama alivyosema Ngombale, tunataka jeshi kubwa zaidi, watu wengi zaidi,” alisema Lowassa.  
 
 

Saturday, December 24, 2016

Penzi la Bibi wa Miaka 60 Laua Kijana wa Miaka 23



KIJANA mwenye umri wa 23 na mpenzi wake, bibi mwenye umri wa miaka 60 , wakazi wa kijiji cha Tentula, Kata ya Ikozi wilayani Sumbawanga, wanashikiliwa na polisi wakihutumiwa kumshambulia na kumuua kikatili jirani yao aitwae Desder Justino (23) kwa kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Inaelezwa kuwa, Justino pia alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na bibi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mauaji hayo yalitokea Desemba 21 mwaka huu saa nne asubuhi katika nyumba ya mwanamke huyo iliyopo kijijini Tentula.

Taarifa kutoka kijijini humo zinadai kuwa, mwanamke huyo licha ya umri wake kuwa mkubwa, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na vijana hao wawili wa rika moja.

Kamanda Kyando hakuwa tayari kutaja majina ya wapenzi hao ambao ni watuhumiwa wa mauaji kwa sababu za uchunguzi.

Lakini alisema mwanaume ana umri wa miaka 23 huku mpenzi wake ana umri wa miaka 60. Akielezea zaidi, Kamanda Kyando alisema siku ya tukio Justino alikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi na kumkuta kijana mwingine (mtuhumiwa), na hapo ndipo ugomvi ukaibuka baina ya vijana hao.Alisema Justino alijeruwa kichwani.

“Wawili hao yaani wapenzi hao (mwanamke na mwanaume) walimshambulia Justino (Desder) kwa kumpiga kichwani na kitu chenye ncha kali na kumjeruhi vibaya na alikufa akiwa anatibiwa hospitalini,” alisema Kamanda Kyando na kuongeza  kuwa, watuhumiwa hao wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani uchunguzi wa awali utakapokamilika.
 
 

Saturday, December 24, 2016

Jaji Magimbi kusikiliza rufaa ya Godbless Lema Desemba 28



JAJI Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa ya kutaka dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Desemba 28 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema rufaa hiyo namba 126 ya mwaka 2016, imepangiwa kusikilizwa na Jaji huyo. Alisema kimsingi wanalalamikia uamuzi wa Mahakama kutomwachia huru, licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpatia dhamana.

Awali, uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, uliweka wazi dhamana.

Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa madai kuwa sheria haizuii kumpa dhamana mtu kwa kesi ya uchochezi, ila kabla ya kutoa masharti ya dhamana licha ya kutamka dhamana ipo wazi, mawakili wa serikali walipinga kumpatia dhamana Lema, kwa madai wameonesha nia ya kukata rufaa.

Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki kama ilivyo na mtuhumiwa asubiri maamuzi ya Mahakama Kuu.

Lema alilazimika kwenda mahabusu hadi sasa katika Gereza Kuu la Kisongo. Baada ya hatua hiyo, mawakili wa Lema wakiongozwa na Sheck Mfinanga, walianza kutafuta suluhisho la mteja wao kupata dhamana na walianza na kuandika maombi na kuitaka Mahakama Kuu kufanya marejeo kwa kuitisha faili la kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Lakini, ombi lilitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi, Novemba 11 mwaka huu kwa madai kuwa walikosea, badala ya kufanya marejeo walitakiwa kukata rufaa. Mawakili hao walilazimika kukata rufaa siku hiyo hiyo na Desemba 2 mwaka huu, ilitupwa na Jaji Fatuma Masengi kwa madai kuwa ilikuwa nje ya muda.

Baada ya hatua hiyo, mawakili hao walipeleka ombi Mahakama Kuu, kuomba kuongezewa muda wa kupeleka notisi ya kukata rufaa yao juu ya dhamana na hatimaye Desemba 20, Jaji Dk Modesta Opiyo, alikubali na kumwongezea muda Lema wa siku 10.

Siku hiyo ya kuongezewa muda, mawakili wa Lema walifanikiwa kukata rufaa hiyo. Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi katika mahabusu ya Gereza Kuu Kisongo.

Alikamatwa Novemba 2 mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na alifikishwa mahakamani Novemba nane mwaka huu, akikabiliwa na mashitaka ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.


Saturday, December 24, 2016

Polisi Yanasa 200 Kwa Ujambazi Dar




JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 200 wanaohusishwa na makosa mbalimbali.

Wanne kati ya hao, wanatuhumiwa kukutwa na gari lililoibwa hivi karibuni katika eneo la ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) zilizopo Manispaa ya Ilala.

Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alitaja watu hao wanne wanaotuhumiwa kukutwa na gari hilo kuwa ni Leonard Said, Omary Said, Shomaly Kilobo na Adam Unemba.

Alisema katika uchunguzi wa awali, watuhumiwa wote wamekiri kuhusika katika wizi wa gari hilo, aina ya Toyota Spacio lenye namba za usajili T 398 CAE, boksi la chuma la kutunzia fedha na televisheni ya ukubwa wa inchi 32.

Alisema Desemba 5, mwaka huu alipokea taarifa kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa TIRA, Egnance Edward (53) kuwa wamekuta ofisi za mamlaka hiyo, zimevunjwa na kuibwa baadhi ya vifaa ikiwemo gari hilo.
 
 

Saturday, December 24, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi Ya Disemba 24



No comments:

Post a Comment